Jumanne, 6 Mei 2014

JESHI LA POLISI LAJIPANGA KUKOMESHA UKATILI NA UNYANYASAJI WA WATOTO.


Na Demetrius Njimbwi - Jeshi la Polisi

Mkuu wa Dawati la Jinsia Nchini Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Adolfina Chialo, amewataka askari wote nchini hususan wale waliopo katika dawati la jinsia kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi ili kukomesha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. 

Hayo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo ya siku tano yanayotolewa kwa Maafisa na askari wa Jeshi la Polisi katika mkoa wa Dar es salaam, ambapo washiriki hao watapatiwa mafunzo ya namna ya kukabiliana na makosa ya ukatili wa kijinsia. 

Kamishna Chialo, alisema kuwa, ili kutokomeza makosa yatokanayo na ukatili wa kijinsia na unyanyasaji kwa watoto, ameihasa jamii kutofumbia macho uovu au aina yeyote ya ukatili na badala yake kuripoti jambo hilo mahala husika au  katika madawati ya jinsia ya Polisi katika kituo chochote cha Polisi  ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa ambapo kwa sasa jumla ya madawati ya jinsia 417 yameanzishwa hapa nchini. 

Kwa upande wake mgeni rasmi wa semina hiyo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii, Bi. Eva Mbilinyi, alisema Kuwa, lengo kuu la mafunzo haya ni kuwasaidia askari Polisi kwa kuwajengea uwezo katika utendaji wao wa kazi na namna sahihi ya kuwahudumia waathirika wa ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto. 

Bi. Eva Mbilinyi, aliongeza kuwa, bila ulinzi, malezi na makuzi sahihi kwa watoto ni wazi kuwa, taifa haliwezi kupiga hatua katika maendeleo hivyo jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa, inamlinda mtoto dhidi ya ukatili wa aina zote za unyanyasaji alisema.

Jumatatu, 5 Mei 2014

SHIRIKA LA NELICO NA MABARAZA YA WATOTO WILAYA YA GEITA WAFANYA ZIARA YA KIMAFUNZO KATIKA SHIRIKA LA KIVULINI

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana la KIVULINI akitoa historia ya shirika la KIVULINI kwa wawakilishi wa mabaraza ya watoto mara baada ya kutembelea ofisi za shirika hilo hapo jana. KIVULINI ni shirika lisolo la kiserikali linalofanya shughuli za kupinga na kutetea Haki za Wanawake na Wasichana katika mikoa yote ya kanda ya ziwa pamoja na mkoa wa Singida tangu mwaka 1999.
Afisa Utetezi na Mitandao ya Kijamii toka Shirika la KIVULINI Bi. Khadija Liganga akifafanua jinsi KIVULINI ilivyoweza kuliinua Shirika la Mtandao la Watoto la Jijini Mwanza (Mwanza Youth and Chidren Network) na kuweza kusimamia na kutetea Haki za Watoto katika jiji la Mwanza. 
Picha ya Pamoja ya Maafisa wa Shirika la KIVULINI, Mkurugenzi na Afisa Mradi wa NELICO, Afisa Maendeleo jamii wa wilaya ya Geita, Muwakilishi wa Plan International pamoja na Wawakilishi wa Mabaraza ya watoto wilayani Geita mara baada ya kumaliza ziara ya Kimafunzo katika ofisi za shirika la KIVULINI.

Shirika la watoto la New Light Children Center Organization (NELICO) la mkoani Geita kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya jamii Geita, limeambatana na wawakilishi 20 toka Mabaraza ya watoto ya kata kumi na moja (11) za wilaya ya Geita kwa ziara ya kimafunzo katika shirika la kutetea Haki za Wanawake na wasichana, KIVULINI la mkoani Mwanza.

Ziara hiyo ya kimafunzo katika shirika la KIVULINI imefanyika hapo jana ikiwa na lengo la kujifunza namna KIVULINI ilivyosaidia Baraza la watoto Mwanza kuweza kuratibu na kutekeleza shughuli zake kikamilifu na kuwa imara zaidi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa NELICO Bi. Paulina Alex alisema kwamba ziara hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa mabaraza ya watoto wilayani Geita juu ya mbinu za kuratibu na kutekeleza miradi mbalimbali lakini pia kujua mafanikio na changamoto za shirika la KIVULINI katika kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika mikoa ya kanda ya ziwa.

“Mabaraza ya watoto ya  Geita bado ni machanga sana na hivyo kufanya safari hii ya mafunzo kuwa ya muhimu sana. Katika safari hii wawakilishi wa mabaraza ya watoto wameweza kupata elimu kubwa kutoka KIVULINI na Baraza la watoto la Mwanza (Mwanza Youth and Children Network) ambalo ni zao la KIVULINI” alisema Bi. Paulina.

Ziara hiyo pia ilikuwa na Bw. Maximillian Kitigwa amabe ni mwakilishi toka shirika la Plan International ambao ni wadau wakubwa wa watoto kwa mkoa wa Geita pamoja na Afisa Maendeleo ya jamii wa wilaya ya Geita Bi. Emma Busanji. Watoto hao pia watafanya ziara katika Mkoa wa Arusha kujionea juhudi za  wadau wa maendeleo katika mkoa huo katika kuwaokoa watoto dhidi ya kufanyishwa kazi hatarishi hasa katika sekta ya madini.

Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea na kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shirika la Kivulini linahamasisha jamii (Wanawake, Wanaume na Vijana) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania. 


Ijumaa, 2 Mei 2014

WASICHANA 30 TOKA WILAYA YA ILEMELA NA NYAMAGANA MWANZA WAPATIWA MAFUNZO YA SIKU TANO KUHUSU ELIMU YA UKATILI WA KIJINSIA MAJUMBANI

Mkurugenzi wa Shiriki la KIVULINI Bw Ramadhan Masele akisisitiza jambo wakati akifunga mafunzo maalum kwa wasichana 30 walio na umri kati ya miaka 18 mpaka 25 kutoka wilaya ya Ilemela na Nyamagana za jijini Mwanza hapo jana. Wasichana hao wamepewa mafunzo kuhusu ukatili wa kijinsia majumbani pamoja na Kingono lengo likiwa ni kuzalisha waelimisha rika wengi zaidi mitaani na kutengeneza jamii isiyokuwa na ukatili wa kijinsia na kingono kwa kwa watoto wa kike.
Mkufunzi wa Masuala ya Kijinsia Bi. Tumaini Kyola akitoa mafunzo kwa kundi la Wasichana 30 ambao hawako mashuleni juu ya mbinu mbalimbali za kuelemisha jamii kuhusu masuala Ukatili wa Majumbani na wa kingono pia. Wasichana hawa wanategemewa kwenda kuwafundisha wasichana wenzao wa mitaani, kila mmoja amepewa lengo la kufikia wasichana 50. 
Baadhi ya wasichana 30 wakiwa makini kufuatilia mafunzo waliokuwa wakipatiwa na mkufunzi wao (hayupo pichani), hili ni kundi la kwanza kwa wasichana waliokuwa nje ya shule ambapo mafunzo ya kundi la pili kwa wasichana waliopo mashuleni yanatarajiwa kuanza mwezi wa sita kwa kushirikisha shule zipatazo 40 toka wilaya za jiji la Mwanza.

Wasichana thelathini pamoja na Mkufunzi wao na baadhi ya maafisa wa Kivulini wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mafunzo hayo ya siku tano hapo jana katika ukumbi wa VETA jijini Mwanza.


Mkurugenzi wa shirika la kutetea Haki za Wanawake na Wasichana KIVULINI lenye makao yake makuu jijini Mwanza Bw. Ramadhan Masele amefunga rasmi mafunzo ya siku tano yanayolenga  kuwajengea wasichana uwezo wa kutoa elimu juu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia chini ya mradi wa kuwashirikisha vijana kuzui Ukatili wa majumbani ikiwa ni pamoja na ukatili wa  kingono kwa watoto wa kike na wasichana.  

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo Bw. Masele aliwataka washiriki wote kutumia elimu hiyo muhimu waliyoipata kutoa elimu na kuongeza uwelewa zaidi kwa jamii yao kuanzia ngazi ya familia, marafiki na vikundi mbalimbali na kuwa chachu ya mabadiliko  juu ya kupigania haki za wanawake na wasichana wanaonyanyaswa kijinsia katika jamii zao.

“Imani yangu ni kuwa semina hii itakuwa ni kiwanda kizuri cha kuwatengeneza nyinyi wote kuwa mabalozi wazuri katika jamii, baada ya mafunzo haya tunaamini kuwa mtakuwa chachu ya mabadiliko katika kutetea na kulinda haki za wanawake na wasichana kwa kukemea, Kupinga, kuripoti na kuzuia aina zote za ukatili wa majumbani na kingono kwa wasichana na wanawake na kutoa taarifa pindi vitendo hivi vinapotokea” alisema Bw. Masele

“Kila mmoja aliyehudhuria mafunzo haya  kwa nafasi aliyonayo tunaamini anaweza kuwa chachu ya mabadiliko endapo atatimiza wajibu wake kwenye eneo analoishi. Hili suala la ukatili wa kijinsia si suala geni nchini hasa eneo hili la kanda ya ziwa hivyo kuna kila sababu ya kuzidisha mapambano dhidi yake, cha muhimu ni kuzingatia mafunzo mliyopewa na muwezeshaji wenu” aliongeza Bw. Masele.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa siku 5 kwa vijana 30 wa kike wenye umri kati ya miaka 18-24 kutoka wilaya mbili za Nyamagana na Ilemela jijini Mwanza. Lengo la Mafunzo ni kuwajengea vijana uwezo wao binafsi na uwezo wa kuelimisha jamii hasa Vijana wenzao  kupambana na kupinga Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika maeneo wanayoishi.

Mafunzo yalianza Jumatatu tarehe 28 Aprili, 2014 mpaka tarehe 2 Aprili, 2014 katika Ukumbi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA kilichopo Nyakato nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Takwimu zinaonyesha bado jamii inakabiliwa na ukatili mkubwa wa kijinsia ambapo ubeberu wa wanaume pamoja na mila na desturi potofu zimeonekana kukandamiza jinsi ya kike zaidi kuliko jinsi ya kiume, ukatili huo ni wa kijamii, kiuchumi pamoja na kisaikolojia hivyo kunaitajika juhudi za dhati na makusudi kuweza kukabiliana na tatizo lilopo kwa jamii.

Akimalizia mawaidha yake kwa washiriki Bw. Masele alisema lengo la mafunzo hayo ni kuona mabadiliko katika mfumo juu ya kujali na kuheshimu haki za mwanamke na wasichana, kwani jamii nyingi zinapambana na mifumo miwili mikubwa, ambayo ni mfumo dume ambao umekuwa ukiwakandamiza wanawake katika jamii na mfumo wa kitabaka unaoongeza nafasi kati ya matajiri na masikini.

Shirika la KIVULINI kwa kushirikiana na Asasi ya Vijana  inayojulikana kama Wadada Centre for Solution Focus Approach ndio waandaji wa mafunzo hayo kupitia mradi wa kuwashirikisha vijana kuzui Ukatili majumbani na Ukatili wa Kingono chini ya ufadhili wa Shirika la terre des hommes ch (tdhschweiz) - Fursa kwa Vijana  la nchini Switzerland

Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na kutetea pamoja na kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shiriki la Kivulini linahamasisha jamii (Wanawake, Wanaume na Vijana ) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.

ASASI TANO ZINAZOPATA RUZUKU TOKA MFUKO WA MSAADA WA KISHERIA (LSF) KWA MIKOA YA KANDA YA ZIWA ZAMALIZA ZIARA YA SIKU 3 SHIRIKA LA KIVULINI

Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Bw Ramadhan Masele akifunga ziara ya kimafunzo ya siku tatu kwa mbele ya washiriki wa ziara hiyo (hawapo pichani), Bw Masele alitoa shukrani kwa maafisa toka mashirika matano ya mikoa ya kanda ya ziwa pamoja na maafisa toka Mfuko wa Msaada wa kisheria (LSF) na Foundation for Civil Society kwa ziara hiyo ya mafunzo.
Mwanakijiji wa kata ya Mwamala Wilaya ya Kwimba Bi. Grace Masanja akieleza msaada wanaopata juu ya elimu na ushauri wa kisheria toka kwa msaidizi wa kisheria katika kata yao, Bi. Grace alitanaibisha kwamba bado kuna tatizo kubwa la unyanyasaji wa kijansia unaofanywa na wanaume dhidi ya wanawake licha ya elimu ya haki za kila jinsi zinatolewa kila siku na kuwaomba wadau wa sheria kuzidisha nguvu kuweza kukomesha tabia za wanaume kupiga wanawake.
Mwanakijiji wa kata ya Mwamala Bw. James Ngosha akiwashukuru wageni toka KIVULINI pamoja na washirika wengine kwa msaada wa kuwapatia muelimishaji wa haki na sheria katika kata yao kwani amekuwa akiwasaidia sana katika kutatua migogoro ya ardhi kijijini kwao.
Maafisa toka Asasi tano za kanda ya ziwa pomoja na wawezeshaji wa KIVULINI, LSF na Foundation for Civil Society wakifanya tathmini ya ziara yao nzima ya siku tatu katika kijiji cha Mwamal baada ya kumaliza ziara ya kutembelea kata za Ngudu, Mwamala na Hungumalwa katika wilaya ya Kwimba.

Maafisa Miradi pamoja na Maafisa Wakaguzi na Tathmini Miradi toka mashirika matano ya Kiraia yanayopata ruzuku kutoka Mfuko wa Msaada wa Kisheria (LSF) Tanzania, yamemaliza ziara ya kimafunzo ya siku tatu katika Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na wasichana Tanzania, KIVULINI la jijini Mwanza, ziara iliyolenga kujifunza na kuboresha ufanyaji kazi wa mashirika hayo kupitia Miradi mbalimbali inayoendeshwa na KIVULINI.

Mashirika hayo matano toka mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mara, na Tabora yalianza mafunzo hayo Jumatatu ya tarehe 28 Aprili, 2014 na kumaliza mafunzo hayo tarehe 30 Aprili, 2014 kwa kutembelea Wasaidizi wa Kisheria wanaofanya kazi ya kutoa elimu na ushauri wa kisheria katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba chini ya shirika la KIVULINI kupitia mradi wa Msaada wa Kisheria unaofadhiliwa na LSF.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa Ziara hiyo Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Bw. Ramadhan Masele aliwashukuru maafisa wote toka mikoa hiyo mitano ya kanda ya ziwa kwa kuhudhuria mafunzo hayo lakini pia aliwashukuru Mfuko wa Msaada wa Kisheria kwa heshima waliyowapa KIVULINI kuwa kituo cha mafunzo kwa asasi nyengine.

“Ziara hii imetoa hamasa nzuri hasa kwa upande wa kimahusiano baina ya Asasi zinazotekeleza mradi wa msaada wa kisheria kwa kanda ya ziwa, pia uzoefu tuliobadilishana kwa siku zote tatu za mafunzo naamini utaenda kuimarisha utendaji kazi wa asasi zetu na kuinua hali ya maisha ya Watanzania kupitia sisi” alisema Mkurugenzi wa KIVULINI Bw Ramadhan Masele.

“Lakini pia tuwashukuru wadau wetu wakubwa katika mradii huu wa msaada wa kisheria, LSF, kwa ubunifu waliouleta wa kutuwezesha kukutana pamoja na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi, na hivyo hivyo shukrani zetu ziende kwa Foundation for Civil Society kwa kushirkiana na SLF kuwa pamoja nasi, tunaomba huu uwe ni mwanzo tu na usiwe mwisho” alimalizia Bw Masele

Ziara hiyo imeratibiwa na LSF kwa kushirikiana na Foundation For Civil Society kutoa hamasa na kuinua utendaji kazi wa Asasi za Kiraia nchini katika kuhakikisha asasi hizo zinatoa matokeo bora katika mradi wa Msaada wa kisheria.



Mashirika yaliyohudhuria ziara hiyo ya Kimafunzo ni Jamii Salama Development Volunteers (JSDV) toka Tabora, Centre for Widows and Children Assistance (CWCA) la mkoani Mara, Mama’s Hope Organization for Legal Aid (MHOLA), Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESHI), Sheria na Haki za Binadamu (SHEHABITA) la mkoani Mara.

WLAC WATOA MSAADA WA KISHERIA NDANI YA KIJIJI CHA MAISHA PLUS

Baadhi ya Washirka wa Maisha Plus 2014 wakitoa mawazo yao katika semina hiyo

Washiriki wa Maisha Plus 2014 wakipewa vijitabu vinavyohusu sheria mbalimbali 

Washiriki wa Maisha Plus wakifuatilia maelezo toka kwa wanasheria (hawapo pichani)

Moja ya kundi toka kwa washiriki wa Maisha Plus wakifanya mjadala 

Mwanasheria toka shirika la Msaada wa Kisheria kwa Wanawake, WLAC
Ikiwa ni siku ya tatu toka Mama Shujaa wa chakula waingie kijijini Maisha Plus na siku ya 37 toka mashindano hayo yaanze rasmi, jopo la Wanasheria kutoka shirika lisilo la kiserikali la WLAC juzi lilitua kijijini hapo kwa ajili ya kutoa mafunzo mbalimbali ya kisheria kwa wanakijiji hao.

Wanasheria hao ambao ni Faudhia Yasin, Sarah Mambea na Juvenile Rwegasira walianza kwa kuwagawa washiriki katika makundi matatu na kisha kuwataka wajadili visa walivyopewa.

Visa hivi vitatu vililenga kupata ufahamu wa wanakijiji juu ya mambo yanayohusiana na Mjane na urithi, sheria ya ndoa na talaka pamoja na ukatili dhidi ya wanawake.

Makundi yawasilisha visa
Kundi la kwanza liliwakilishwa na washiriki Mbonimpaye Nkoronko kutoka Mtwara, Boniphace Meng’anyi kutoka Dar es salaam na Ngabonziza Daniel kutoka nchini Rwanda. Vijana hawa katika kisa chao waligundua kwamba mtu akishakuwa katika ndoa kwa muda wa miaka mitatu tayari anakua mwanandoa halali.

Kundi hili lilitoa mapendekezo ya kutolewa kwa elimu juu ya masuala ya ndoa kabla ya watu kuingia katika ndoa na uwepo wa sheria za kuondoa ukatili na kuleta usawa katika jamii zetu. Boniphace alisisitiza kwamba uwepo wa sheria madhubuti ndio mkombozi pekee wa wanyonge kwani bila hivyo watu walio matajiri wanapendelewa.

Mshiriki Ally Thabit kutoka Mwanza alichaguliwa kutoa mrejesho wa kundi namba mbili ambao kisa mkasa chao kilimuhusu Bwana Musa ambaye alifungua akaunti tatu za siri na pia kujenga hoteli kisiri bila mkewe kufahamu, kisa hicho mwishoni kinaonyesha Bwana Musa alifariki ghafla na hivyo kuleta msuguano mkali sana katika familia yake kuhusu mgawanyo wa mali.

Huku akijibu maswali ya mirathi yaliyojitokeza katika kisa hicho Ally anataja, miongoni mwa hasara nyingine, kwamba kwanza haki ya urithi imepotea, pili usiri wa baba umekuwa kikwazo katika familia kupata haki ya msingi lakini tatu kwamba huenda wakati Bwana Musa anafariki kulikuwa na pesa nyingi katika akaunti yake benki ambazo zingeisaidia familia yake ambayo kwa mujibu wa kisa hicho hivi sasa familia hiyo inakumbwa na janga kali la umaskini.

Katika kuelezea umuhimu wa wosia; Ally aliendelea kusema kwamba wosia huondoa utata inapotokea kifo na vilevile wosia huondoa chuki na fitna baina ya ndugu na jamaa.

Mwanamke anaweza kuwa msimamizi wa mirathi
Naye Faudhia Yassin ambaye ni mratibu wa kampeni ya TUNAWEZA kutoka WLAC aliwaeleza wanakijiji kwamba Mwanamke amekuwa akitengwa sana katika ugawaji mali hivyo ni muhimu jamii kutambua kwamba hata wanawake waliofiwa na waume zao wanaweza kuwa wasimamizi halali wa mirathi.

Faudhia alisema ikitokea baba amefariki, familia ichukue cheti cha kifo na kukipeleka mahakamani kuomba mahakama imuidhinishe waliyempendekeza kuwa msimamizi wa mirathi.

Ndoa halali ni ipi?
Kundi la tatu liliwakilishwa na Mama Shujaa wa chakula Grace G.D. Mahumbuka kutoka Kagera pamoja na vijana wa Maisha Plus ambao ni Bakari Khalid kutoka Shinyanga na Said Kawawa kutoka nchini Uganda.

Kundi hili liligundua kwamba mtoto wa kike hathaminiki kama ilivyo kwa mtoto wa kiume, lakini elimu pia ya uelewa juu ya mambo ya haki ni duni. Sehemu ya kisa hicho iliwataja watu wawili wa jinsia tofauti walioishi pamoja kwa kipindi cha miaka 12 bila kuwa na ndoa hata ya kimila.

Aidha kundi hili lilipendekeza sheria ya ndoa ya Tanzania iboreshwe na kwamba ifahamike kuwa mtoto wa kike ana haki ya kurithi sehemu ya mali ya wazazi wake sawa sawa na ilivyo kwa mtoto wa kiume.

Waliendelea kwa kushauri kwamba inapotokea tatizo katika ngazi ya familia baina ya mke na mme basi aliyetendewa ukatili ajaribu kusuruhisha katika ngazi ya familia ikishindana basi aende katika ustawi wa jamii, baraza la kata, ofisi za ushauri wa kisheria za mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali kama itashindikana kote huko basi mwisho achukue hatua za kisheria za kimahakama.

Akifafanua kuhusu hoja hii, Mwanasheria Juvenile Rwegasira kutoka WLAC alisema kwamba watu wawili wa jinsia tofauti wakiishi pamoja kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo na jamii ikafahamu kwamba hawa ni mme na mke, hiyo kisheria inaitwa dhana ya ndoa.

Mwanasheria Rwegasira alisisitiza kwamba ni lazima iwe miaka miwili mfululizo na sio ile ya kuja miezi miwili na kuondoka na kuja tena na kuondoka.

Hata hivyo, Bw. Rwegasira alitoa angalizo kwamba ndoa hii ni rahisi sana kukanushika hivyo akasisitiza umuhimu wa kuhitaji tamko la Mahakama kuidhinisha dhana ya ndoa.

Akiendelea Bw. Rwegasira alisema kwamba ndoa hii ni ya kienyeji mno na haina cheti hivyo ikitokea mmoja amefariki inaleta shida sana kwenye ugawaji wa mali.

Pata msaada wa kisheria BURE
WLAC ni kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake. Kwa wenye matatizo ya Mirathi, Ndoa, Ardhi, Elimu, Ajira, Matunzo ya Watoto na Mengineyo wapige simu BURE kwenda namba 0800780100

Jumanne, 29 Aprili 2014

HALMASHAURI NA WADAU WA JIJI LA MWANZA WAANZA MAANDALIZI YA SHEREHE ZA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA JUNI 16.

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi inayoundwa na wadau wa watoto jijini Mwanza Bw. Godfrey Salumu akifafanua utaratibu mzima wa utendaji kazi wa kamati ndogo ndogo zilizoundwa kwa wajumbe (hawapo pichani) ili kuweza kufanikisha maadhimisho hayo.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya jiji la Mwanza Bi Eluminata Mwita akisikiliza jambo kwa makini toka kwa wajumbe (hawapo pichani). 

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana, KIVULINI Bw Ramadhani Masele (kushoto) ambae pia ni mjumbe wa kamati ya ndogo ya Uratibu, Mipango na Fedha akiteta jambo na mjumbe mwenzake wakati wa kikao hicho.

Wajumbe wa Kikao cha kwanza cha maandalizi ya Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika itakayofanyika Juni 16 chini ya kauli mbiu ya “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto ni Jukumu Letu Sote”. 

Uongozi wa kamati ya maandalizi ya sherehe ya siku ya Mtoto wa Afrika wilaya ya Nyamagana, Mwanza. Kulia ni Bw Godfrey Salumu ambae ni Mwenyekiti wa kamati, Bw. Devis Mrope (katikati) ambae na Katibu, kushoto ni Katibu Msaidizi Bi. Francisca Michael.

Halmashauri pamoja na wadau toka mashirika na taasisi za kutetea na kulinda haki za watoto jijini Mwanza wameanza rasmi vikao vya maandalizi ya kuadhimisha sherehe za siku ya mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Mwaka Juni 16.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri wa Jiji la Mwanza chini ya Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Bi. Eluminatha Mwita wajumbe walikubaliana kuadhimisha siku hiyo katika Kata ya Buhongwa, kwa Wilaya ya Nyamagana.

Siku ya mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu, na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanywa kila juni 16 tangu ilipotangazwa kuwa siku rasmi mwaka 1991 na jumuiya ya umoja wa Afrika.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho Afisa Maendeleo Jamii wa Jiji la Mwanza Bi. Eluminatha Mwita alisema kuwa kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Kuondoa Mila Zenye Kuleta Madhara kwa Watoto ni Jukumu Letu Sote” na kufafanua kuwa kauli hiyo inalenga kuwasisitiza wazazi na walezi kuacha mila potofu zenye kuleta madhara kwa watoto.

Bi Eluminatha alisema kuwa “Kauli mbiu hiyo ina lenga kuangalia mila zote kandamizi na potofu zinazotokana na jamii husika katika malezi ya mtoto na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa watoto wa mitaani, kubakwa kwa watoto, kukosa elimu, afya na malezi bora pamoja na vifo kwa watoto hawa”.

Kikao hicho cha kwanza kiliweza kuchagua viongozi wa kamati hiyo ya maandalizi, mwenyekiti aliyechaguliwa ni Godfrey Salum huku katibu ni Devis Mrope na katibu msaidizi akichaguliwa Francisca Michael, baada ya kupata viongozi kamati nne ziliundwa na wajumbe, Kamati ya Uratibu, Mipango na Fedha, Kamati ya Usafiri na Ulinzi, Kamati ya Mapambo na Burudani pamoja na kamati ya Hotuba na Habari.

Imeandaliwa na Afisa Habari wa Kamati ya Maandalizi
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika - Mwanza
Hassan Mrope

0713441892